Baada ya Okwi; Kaseja, Niyonzima, na ‘Chuji’ hawapo kambini Yanga



YANGA SC imeingiza wachezaji 20 kambini eneo la Bahari Beach kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu, Simba SC kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kukamilisha msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa taarifa ya kwenye tovuti ya klabu hiyo leo, wachezaji walioingia kambini ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Ibrahim Job, Rajab Zahir, Kevin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, wakati viungo ni Frank Domayo, Hassan Dilunga, Salum Telela, Hamisi Thabit na Nizar Khalfan na washambuliaji ni Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa, Jerry Tegete, Hamisi Kiiza, Hussein Javu na Simon Msuva.


Bado hazijulikani sababu za wachezaji Juma Kaseja,Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Athumani Iddi ‘Chuji’ na David Luhende kutokuwa kambini tangu baada ya mechi na JKT Mgambo Yanga wakilala 2-1 Tanga.
Kocha Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm amekaririwa na tovuti hiyo akisema vijana wake wapo katika hali nzuri kuelekea mchezo wa Jumamosi, kwani hakuna majeruhi hata mmoja kati yao.
Amewasifu wanazidi kuonyesha mabadiliko makubwa kiuchezaji, mafunzo yake wanaonekana kuyaelewa vizuri hivyo kikubwa anaomba waendelee kuwa katika hali nzuri kuelekea mchezo na ana imani kikosi chake kitaibuka na ushindi.
“Nina uzoefu na michezo ya watani wa jadi, huwa inakua migumu kwa kila timu kutokana na kila timu kutaka kuonyesha wapenzi, washabiki na wanachama wake kuwa wako vizuri, Simba ni timu nzuri, lakini bado sioni kikwazo cha kutuzuia tusiibuke na ushindi katika mchezo huo,’alisema.
Leo jioni kikosi kitafanya mazoezi katika Uwanja wa Bko Beach Veterani ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo huo.
Yanga SC imeshindwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu, baada ya kuzidiwa kete na Azam FC iliyofikisha pointi 59 ikiwa na mechi moja mkononi ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yeyote.
Yanga SC itafikisha pointi 58 ikifanikiwa kuifunga Simba SC ambayo imeweka kambi visiwani Zanzibar tangu jana kwa ajili ya mchezo huo.

0 comments:

Post a Comment