PAZIA la ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014 linafungwa kesho aprili 19 kwa timu zote 14 kushuka uwanjani katika miji tofauti nchini.
Ligi inamalizika kesho wakati timu tatu zimeshajihakikishia nafasi tatu za juu.
Azam fc wametwaa ubingwa baada ya kufikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na klabu yoyote.
Yanga wamechukua nafasi ya pili wakiwa na pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote chini yake.
Mbeya City nao wameshika nafasi ya tatu kwa pointi 46 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ya chini yake.
Simba sc wao wao wapo mbioni kuisaka nafasi ya nne kwa pointi zao 37 baada ya kucheza mechi 25.
Nafasi ya tano wapo Kagera Sugar wenye pointi 35, na endapo Simba watafungwa kesho na wao wakashinda, basi Mnyama anaweza kumaliza ligi katika nafasi ya tano.
Katika mechi zote 7 hapo kesho, mechi tatu pekee zina hamasa kubwa kwa mashabiki wa soka nchini.
Mechi ya kwanza iliyovuta hisia za mashabiki wa soka ni ile ya Yanga dhidi ya Simba sc ndani ya uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Timu hizi zitakutana zikiwa na mafanikio tofauti msimu huu ambapo Yanga wameambulia nafasi ya pili, huku Mnyama akijikongoja katika nafasi ya nne.
Simba na Yanga zinakutana jumamosi, huku Yanga wakiwazidi wenzao kwa mafanikio msimu huu.
Yanga wamecheza mechi 25 sawa na Simba sc, lakini wameweza kushinda mechi 16, kutoa sare 7 na kufungwa mechi 2 tu, hivyo kufikisha pointi 55 katika nafasi ya pili.
Pia Yanga ndio klabu iliyofunga mabao mengi zaidi mpaka sasa ambapo imetikisa nyavu za timu pinzani mara 60, lakini wamefungwa mabao 18 na kuwa timu ya pili kufungwa mabao machache.
Mabingwa watetezi Azam fc wamefunga mabao 50 na kufungwa mabao 15 tu, hivyo kuwa timu yenye rekodi ya kufungwa mabao machache zaidi msimu huu.
Ukirejea kwa upande wa Simba sc, msimu huu upepo mbaya umevuma kwa upande wao kwasababu mpaka sasa wamecheza mechi 25 na kushinda mechi 9, sare 10 na kufungwa mechi 6.
Pia Mnyama Simba amefanikiwa kufunga mabao 40 na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara 26, huku wakiiwinda nafasi ya nne.
Mechi ya kesho haina jipya zaidi ya klabu hizo kulinda heshima tu.
Hata Yanga wakishinda hawana uwezo wa kusogea juu, labda Simba wanaweza kujihakikishia nafasi ya nne msimu huu endapo wataibuka na ushindi.
Mechi ya watani huwa inavuta hisia za mashabiki wengi wa soka, hivyo tusubiri kuona nani ataibuka kidedea.
Mechi ya pili yenye mvuto ni ile ya Ashanti United dhidi ya Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Timu hizi zitapambana ili kupata timu moja itakayoshuka daraja msimu huu.
Timu zote zina pointi 25 baada ya kucheza mechi 25, lakini Prisons wanawazidi wenzao kwa wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Matokeo mazuri kwa Ashanti ni ushindi tu, kwasababu wakifungwa au kutoa sare watakuwa wameungana na JKT Oljoro na Rhino kushuka daraja.
Sare kwa Prisons au ushindi itakuwa faida kwao na wataendelea kudunda ligi kuu msimu ujao.
Hii ni mechi tamu mno kwasababu makocha wa klabu hizi, Abdallal Kibadeni ( Ashanti) na David Mwamwaja (Prisons) wataingia uwanjani wakiwa na malengo sawa.
Wote walipewa timu mzunguko huu wa pili ili kuzinusuru zisishuke daraja, lakini siku ya mwisho wanakutana pamoja.
Kibadeni ndiye mwenye shughuli pevu kwasababu yeye anahitaji ushindi tu, wakati mwenzake anahitaji hata sare.
Mechi ya tatu kwa mvuto ni baina ya mabingwa Azam fc dhidi ya JKT Ruvu ndani ya uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Hii haina presha yoyote, lakini uzuri wake unatokana na uhitaji wa matokeo kwa Azam fc ili wabebe `ndoo` ya ligi kuu bila kufungwa timu yoyote.
Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog alisema anahitaji kuchukua ubingwa kwa kushinda mechi zote, hivyo aliwataka wachezaji wake kucheza kwa makini dhidi ya JKT Ruvu hapo kesho.
Mechi nyingine za kesho ni baina ya Wagonga Nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc dhidi ya Mgambo JKT kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya sokoine jijini Mbeya.
Vibonde wa ligi hiyo walioshuka daraja, Maafande wa Rhino Rangers watawakaribisha Ruvu Shooting katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.
Timu nyingine iliyoshuka daraja, JKT Oljoro itakuwa mwenyeji wa mabingwa wa zamani wa Tanzania , mwaka 1999 na 2000, Mtibwa Sugar katika uwanja wa Shk. Amri Abeid Kaluta, jijini Arusha.
Wagosi wa kaya, Coastal Union watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
CHANZO: SHAFFIH DAUDA.
0 comments:
Post a Comment