RAMSEY MAJERUHI TENA

 
MSIMU tofauti, lakini shetani yuleyule. Wakati Arsenal iliathiriwa sana na majeruhi msimu uliopita, msimu huu hadithi inaweza kuwa ileile. Kiungo wao mahiri, roho ya timu kwa sasa, Aaron Ramsey anaweza kulikosa pambano dhidi ya Man City keshokutwa kwa kuwa ni majeruhi.
Ramsey, 23, aliumia kifundo cha mguu wake katika pambano kati ya timu yake ya taifa, Wales dhidi ya Andorra juzi ambalo timu yake ilishinda mabao 2-1 yote yakifungwa na staa wa Real Madrid, Gareth Bale.
Katika dakika ya 89 ya mchezo staa huyo alitolewa uwanjani na jana alitazamiwa kupimwa kama angeweza kucheza katika pambano dhidi ya Manchester City linalotazamiwa kuchezwa Jumamosi mchana.
“Aaron aligongwa kidogo mguuni na akajikunja vibaya katika kifundo cha mguu. Ilikuwa mwishoni mwa mechi na hakukuwa na maana tena kuendelea kumchezesha. Ni matumaini atakuwa tayari kwa ajili ya Arsenal mwishoni mwa wiki, lakini itabidi tumtazame katika saa 24 au 48 zijazo,” alisema kocha wa Wales, Chris Coleman.
Kama alivyoanza katika msimu uliopita, msimu huu tayari Ramsey ameuanza kwa kuwa fomu akifunga mabao mawili katika mechi tatu za Ligi Kuu ya England na alikuwa silaha kubwa kwa timu yake ya Wales katika pambano la juzi licha ya mabao kufungwa na Bale.
Msimu uliopita, Arsenal ilikosa kasi baada ya kuumia kwa Ramsey ambaye alikuwa katika fomu na kama akikosekana tena kocha Arsene Wenger atakuwa katika wakati mgumu wakati huu akisaka taji la Ligi Kuu ya England kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004.
Kama vile haitoshi kuna wasiwasi kuwa huenda Arsenal pia ikamkosa staa mwingine, Mesut Ozil ambaye aliumia katika pambano la mwisho la Arsenal dhidi ya Leicester City na alikosa mechi ya kufuzu michuano ya Euro 2016 dhidi ya Scotland ambayo Ujerumani ilishinda magoli 2-1.
Baada ya pambano gumu dhidi ya Man City katika Uwanja wa Emirates Jumamosi, Arsenal watasafiri mpaka Ujerumani kwa ajili ya kucheza pambano la kwanza la makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund.

0 comments:

Post a Comment