Shujaa; David Luiz akishangilia baada ya kufunga bao la pili dhidi ya Colombia |
Beki David Luiz kwa mara nyingine alikuwa shujaa wa Brazil baada ya kufunga bao la pili dakika ya 69 kwa shuti kali la mpira wa adhabu kutoka nje kabisa ya boksi.
Nahodha Thiago Silva alitangulia kuifungia Brazil bao la kwanza dakika ya saba, lakini bahati mbaya kwake akaonyeshwa kadi ya pili ya njano kwenye mashindano haya, ambayo itamfanya akose mchezo wa Nusu Fainali.
Nyota wa Brazil Neymar kwa mara nyingine alikuwa chini ya ulinzi mkali, akichezewa rafu nyingi, wakati nyota wa Colombia, James Rodriguez pamoja na kuchungwa mno na mabeki wa wenyeji, lakini alifanikiwa kuifungia timu yake bao la kufutia machozi kwa penalti dakika ya 80.
Penalti hiyo ilitolewa na refa wa Hispania, Carlos Velasco Carballo baada ya kipa Julio Cesar kumkwatua Rodriguez wakati anaenda kufunga baada ya kufanikiwa kuibomoa ngome ya Brazil.
Brazil sasa itakutana na Ujerumani katika Nusu Fainali, ambayo mapema leo imeitoa Ufaransa kwa bao 1-0 mjini Rio.
Kikosi cha Brazil kilikuwa; Julio Cesar, Maicon, Thiago Silva, Luiz, Marcelo, Fernandinho, Paulinho, Oscar, Neymar, Hulk/Ramires dk82 na Fred.
Colombia: Ospina, Zuniga, Zapata, Yepes, Armero, Guarin, Sanchez Moreno, Cuadrado, Rodriguez, Ibarbo/Ramos dk46 na Gutierrez.
0 comments:
Post a Comment