MWANAMUZIKI MKONGWE WA TWANGA PEPETA AFARIKI DUNIA

Amigolas enzi za uhai wake

Amigolas akiwa na Twanga Pepeta
MWANAMUZIKI wa  zamani wa Bendi ya African Stars International ‘Twanga Pepeta’, Khamis Kayumbu ‘Amigolas’  amefariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya kulazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa siku kadhaa.
Amigo alilazwa Muhimbili kwa matatizo ya moyo ambapo taratibu za kufanyiwa upasuaji zilikuwa zikiandaliwa lakini mauti yakamkuta kabla ya lolote kufanyika.
Mwimbaji huyu ambaye hadi anafariki, alikuwa mtumishi wa bendi ya Ruvu Stars inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Amigo alikuwa mmoja wa wanamuziki waasisi wa Twanga Pepeta, akaitumikia kwa uaminifu mkubwa kwa miaka mingi kabla ya mwanzoni mwa mwaka huu yeye na wenzake kadhaa kuanzisha Super Stars Band ambayo baadae ikachukuliwa na JKT na kuwa Ruvu Stars Band.
Akiwa Twanga Amigo akajijengea umaarufu wa aina yake na kuwa kama moja ya nembo ya bendi, katika utumishi wake uliotukuka ndani bendi hiyo, akafanikiwa kutunga wimbo mmoja 'AMINATA'  ambao ulikamata chati kwa miaka mingi tangu ulivyorekodiwa mwaka 2003.
Kufariki kwa Amigo ni pengo kubwa kwa Ruvu Stars hasa kutokana na ukweli kuwa yeye ndiye alikuwa
‘injinia’ wa mipango yote kuanzia Super Stars hadi Ruvu.
Kabla ya Twanga Pepeta, Amigo aliitumikia pia bendi ya Bicco Stars chini ya Kinguti System.
Msiba uko nyumbani kwa mama mzazi wa marehemu Mburahati jijini Dar es Salaam jirani kabisa na Shule ya Msingi Mianzini na taratibu za mazishi zinasubiri ndugu na jamaa kutoka Tabora na Kigoma.

0 comments:

Post a Comment