MTIBWA 2-0 MBEYA CITY: MASHABIKI WACHARUKA

Wakata Miwa wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar, wameendeleza wimbi la ushindi na kubaki kuwa timu pekee ambayo haijafungwa katika Ligi Kuu, baada ya kuizabua Mbeya City ya kwa mabao 2-0 katika pambano kali kwenye Uwanja wa Sokoine.
Ushindi huo umewaweka juu zaidi Mtibwa Sugar kwa toafuti ya pointi tatu, baada ya kuifanya kufikisha pointi 13, huku ikiziacha Yanga na Azam FC zikibanana katika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 10 baada ya mechi tano tano kwa kila kikosi tangu kuanza kwa msimu huu wa 2014/15.
Bao la kwanza la Mtibwa Sugar lilifungwa dakika ya 20 na nyota wake Ame Ally, akiunganisha kona iliyopigwa na beki wa kushoto wa zamani wa Yanga anayekipiga na ‘Wakata Miwa’ hao kwa sasa, David Luhende. Baada ya bao, Mtibwa waliendelea kuishambulia Mbeya City na nusura wapate bao la pili dakika ya 31 kupitia Ally Shariff.
Mbeya City walipigana kadri walivyoweza kujaribu kusawazisha bao hilo, lakini juhudi zao hazikuzaa matunda, hivyo hadi mapumziko, matokeo yalikuwa wageni kuongoza mechi kwa bao hilo 1-0 dhidi ya wenyeji wao ambao msimu huu unaonekana kuwa mgumu kwao.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ya aina yake Mbeya City wakipania kusawazisha bao, ambako walianza na badiliko la kumtoa Themi Felix na nafasi yake kuchukuliwa na Peter Malyanzi, ambaye nusura aipatie timu yake bao la kusawazisha, lakini shuti lake dakika ya 53 lilidakwa na kipa wa Mtibwa Said Mohammed.
Dakika ya 76, Mtibwa wakajihakikishia ushindi muhimu, kutokana na bao maridadi la Andrew Vicent, alilofunga baada ya kuwalaamba chenga mabeki wa Mbeya City na kufumua shuti kali na kumshinda kipa David Burhani.

Dakika moja kabla ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi Hashimu Abdallah wa Dar es Salaam, Mtibwa nusura wapate bao la tatu, lakini shuti la adhabu ndogo nje ya boksi, iliyotokana na Vicent kuchezewa rafu, kupaa nje ya lango Hadi mwisho, Mbeya City sifuri, Mtibwa Sugar mabao 2-0.

Mashabiki wa Mbeya City ambao awali walikaribia kulishambulia basi la Mtibwa Sugar baada ya wageni hao kupata bao la pili, baada ya mechi kwisha waliwalazimisha wachezaji wa timu yao kutopanda gari la timu yao, badala yake watembee nao pamoja kwa miguu kwenda Hosteli wanakoishi, ikiwa ni ishara ya kuwaunga mkono licha ya kipigo.

Vikosi katika pambano hilo vilipangwa hivi, Mbeya City: David Burhani, Kenny Ally, Hassan Mwasapili, Deogratius Julius, Yohana Morris, Yusuph Abdallah, Deus Kaseke, Steven Mazanda, Paul Nonga, Saad Kipanga na Themi Felix.

Mtibwa Sugar: Mtibwa Sugar, Said Mohammed, David Luhende, Salim Mbonde, Andrew Vicent, Shabani Nditi, Mussa Hassan ‘Mgosi’, Mohammed Ibrahim, Ame Ally, Mussa Nampaka na Ally Shariff.

Credits:Hivisasa.co.tz

0 comments:

Post a Comment